Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe
31 Oktoba, 2016 ataanza ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya
kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Rais
Magufuli anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya saa nne asubuhi na baadaye
kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi
ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.
Pamoja
na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda
kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo
Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na
mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu Jijini Nairobi
Katika
ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha
Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua
barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.
Barabara
hiyo mchepuko ya Southern By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya
barabara nchini Kenya, inaunganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi
kwa barabara za juu na chini na imejengwa kwa lengo la kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji hilo.
Rais Magufuli anatarajiwa kumaliza ziara yake tarehe 01 Novemba, 2016 na kurejea Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
0 Comments
on