Header Ads Widget

Makonda kuwatimua watumishi wa ardhi Dar waliokaa kwenye idara zao kwa zaidi ya miaka 5

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hataki kuwaona watumishi wa ardhi katika manispaa za Dar es salaam ambao wamekaa kwenye nyadhifa hizo kwa zaidi ya miaka 5 kutokana na kuwa na mtandao ambao unasababisha matatizo mengi kwa Wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na wananchi

Akiongea katika ziara yake Jumatano hii akiwa Pugu Kajiungeni Ilala Jijini Dar es salaam, Makonda alisema atawashughulikia maafisa ardhi ambao wameshindwa kuwatumikia Wananchi kama walivyoagizwa.
Alifikia uamuzi huo, baada ya malalamiko ya wananchi dhidi ya idara ya ardhi kuwa mengi na maofisa wa idara hiyo, kushindwa kuyatolea ufafanuzi yakanifu.
Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilala, Emmanuel Richard alishindwa kutoa ufafanuzi juu ya mgogoro wa ardhi unaohusu wananchi waliohamishiwa eneo la Pugu Mwakanga kutoka Kipawa ili kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), zoezi ambalo lilitekelezwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Wakati Richard akishindwa kujieleza, Afisa Upimaji Ardhi wa manispaa hiyo Ramadhani Selemani naye alishindwa kueleza kiundani juu ya mgogoro huo, hali iliyo mkera Makonda.
Selemani alisukumia mpira TAA kuwa ndiyo inahusika na suala hilo, hali iliyomfanya Makonda kumpigia simu moja kwa moja Mkurugenzi wa TAA huku akiwa ameweka sauti kubwa ‘roud speaker’ mbele ya wananchi, ambapo mkurugenzi huyo alijibu kuwa alikwisha mtuma afisa wake kuwepo katika mkutano huo ili kujibu hoja ingawa hakuwepo kwa wakati huo.
Aidha wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuporwa ardhi na watu wenye fedha, kubadilishiwa hatimiliki au namba za maeneo yao bila kushirikishwa, kudhurumiwa fidia zao pindi wanapohamishwa kupisha miradi na nyaraka zao kupotezwa kwa maksudi katika ofisi za idara hizo.
Kufuatia hali hiyo, Makonda alisema mtendaji yeyote ambaye amekaa katika idara ya ardhi na mipango miji kwa zaidi ya miaka mitano atahamishwa ili kuvunja mtandao wa uovu ulipo wa maofisa hao.
“Pamoja na kwamba Mungu anawaona mimi nitashughulika na nyinyi.Tumechoka kuwa na kero za ardhi zisizo na kikomo.Nyie oneni raha kutembea huku mkijimwayamwaya na matumbo yenu wakati wananchi wanateseka na kuishi kwa dhiki kwa sababu yenu,”alisema Makonda huku akionyesha kukerwa .
Aliongeza, ”Watu wote mliokaa kwenye Idara za ardhi kwenye manispaa zote za mkoa wa Dar es salaam mtaondoka. Mmejijengea mitandao na njia zenu mnazo tumia kula mwisho wa siku kila kunapokucha ni migogoro ya ardhi wananchi wanabaki kuteseka . Tunataka migogoro hiyo iishe,”

Post a Comment

0 Comments