Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali
imekwishapeleka zaidi ya sh. bilioni 177 kwenye halmashauri mbalimbali
nchini ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo jana
(Alhamisi, Novemba 3, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali
lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka
kupata kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya
maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini.
“Kwa
kuwa Serikali ina mifumo, miongozo, sheria na taratibu za kupeleka
fedha kwenye halmashauri mara baada ya kikao cha bajeti. Mheshimiwa
Waziri Mkuu unatoa kauli gani kuhusu ucheleweshwaji wa fedha hizo katika
halmashauri nchini zikiwemo za mkoa wa Tabora? Alihoji Mheshimiwa Munde.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema:
“Baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha,
Serikali ilianza kujiridhisha uwepo wa mfumo sahihi ya makusanyo na
mapato na matumizi yake. Ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya kikao
cha bajeti inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha
zilizopangwa.”
Waziri
Mkuu alisema Serikali ilianza kupeleka watumishi watakaosimamia
ukusanyaji mapato katika halmashauri zote nchini. Kutathmini miradi yote
iliyoanza ambayo haijaendelezwa pamoja na mipya ili kutambua thamani na
kisha kupeleka fedha.
Alisema
Serikali itaendelea na upelekaji wa fedha kwenye halmashauri kwa ajili
ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Alizisisitiza halmashauri hizo
kuendelea kukusanya mapato ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha
wanazopelekewa na watumie mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato
hayo.
Aidha,
Waziri Mkuu alizitaka halmashauri zote nchini zihakikishe fedha
zinazopelekwa katika maeneo yao zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa
miradi husuka. Aliwasihi Wabunge wafuatilie na wasimamie matumizi ya
fedha hizo ili miradi iliyopangwa iweze kukamilika.
Wakati huo huo;
Waziri Mkuu alisema Serikali haijafilisika na kuhusu suala la mfuko wa
jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge
watajulishwa kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya
maendeleo.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la
Ukonga Mheshimiwa Mwita Waitara aliyetaka kupatiwa kauli ya Serikali
kuhusu kutopelekwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.
Pia
Mheshimiwa Waitara alilalamikia kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha
kidogo katika mgawo wa mfuko wa jimbo ambazo ni sh. milioni 16 licha ya
kuwa na wananchi wengi huku jimbo la Segerea alilosemma lina watu
wachache likitengewa sh. milioni 33. Aliiomba Serikali ingalie upya
ugawaji huo kulingana na mazingira ya jimbo husika.
Waziri
Mkuu alisema kumejitokeza matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo
zaidi ya moja na Serikali inaendelea kufanya sensa kutambua idadi ya
wananchi kwenye majimbo hayo ili itakapopeleka fedha iweze kuzingatia
idadi hiyo na kuwawezesha wabunge kupanga miradi ya maendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 Comments
on