Kusimamia ukurasa wa biashara wa Facebook au Instagram si lelemama.
Unahitaji kuwa mbunifu kwelikweli.
Unahitaji kuendelea kuwavutia watu na wateja wako kuendelea kuutembelea ukurasa wako wa biashara.
Mojawapo ya njia bora kabisa ya kuwavutia watu katika biashara kwa kutumia mitandao ya kijamii ni matumizi ya habari picha –visual content.
Si rahisi kuendelea kuandaa na kupakia habari picha zinazowafanya watu waendelee kutoa maoni, ku-LIKE au ku-SHARE.
Habari picha ni za lazimakatika mitandao ya kijamii.
Lakini inakuhitaji kujua mambo mengi ili kuweza kumudu kuandaa habari picha zinazovutia. Itakuhitaji kufahamu mambo kama vile rangi, muundo wa herufi (fonts), na usanifu. Pia itakuhitaji kulipia fedha (katika dollar) ili kuweza kupata baadhi ya programu zinazohitajika.
Pamoja na haya yote, bado unaweza kutengeneza habari picha zinazovutia sana.
Katika makala hii nitakufundisha ‘kwa nini’ na ‘jinsi ya’ za kuandaa picha na habari picha za ukweli kwa ajili ya kurasa zako za mitandao ya kijamii.
Utaweza kutumia picha na habari picha katika maeneo kama vile:
  • Katika maandiko yako kwenye tovuti ya biashara
  • Kurasa za mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter, n.k
  • Kuandaa na kuonesha nukuu (quotes) mbalimbali
  • Kuonesha kwa picha maana ya mambo mbalimbali kama vile apps

Kwa nini unatakiwa kutumia picha na habari picha katika biashara yako

Picha na habari picha (graphics) ni sehemu muhimu na uti wa mgongo wa mawasiliano katika ulimwengu wa digitali.
Ni kwa sababu husaidia kwa kiasi kikubwa kujenga jina na ushawishi kwa watu wanaoona, kusoma, na kusikiliza juu ya bidhaa au huduma ulizonazo. Ni sehemu muhimu ya mpango mkakati wa kujitangaza kibiashara.
Picha na habari picha zinahitajika kwa ajili ya:
  • Kuandaa vipeperushi
  • Kuandaa maudhui katika mitandao ya kijamii (social media posts)
  • Kuandaa kadi za biashara (business cards)
  • Kuandaa matangazo
  • Kuandaa mwaliko
  • Kuandaa dokumenti za kufunza watu (presentations)
Kwa hivyo mjadala si uhitaji wa picha na habari picha, bali ni kwa namna gani utaweza kuandaa na kuzionesha kwa wateja na watu wote. Na tena bila ya kutumia fedha nyingi au muda mrefu sana.
Picha na habari picha ndizo zinazopelekea watu kuwa na hamu ya kusoma ulichokiandika. Hupelekea wateja wako kuendelea kukuunga mkono pale unapotangaza bidhaa mpya.
Picha na habari picha huwafanya watu kusambaza ujumbe kwa wengine. Picha na habari picha huvutia machoni na kuwafanya watu ‘kuamshwa’ kihisia.

Ufanyeje ili kutengeneza picha na habari picha maarufu?

Nini basi kinapelekea picha au habari picha kupendwa na watu?
Kuna picha na habari picha ambazo ni za kupendeza sana kiasi kwamba husambaa kwa haraka katika wavuti kama moto wa nyika. Na kuna zile ambazo ni za kawaida sana na ambazo zinavutia watu wachache tu.
Ni nini ambacho kinapelekea picha au habari picha kuwa na mvuto?
Ili kufahamu undani wa swala hili, tuanze kwa kuona mambo kadhaa ambayo hupelekea picha au habari picha kusambaa kwa kasi na kupata LIKES au SHARES nyingi katika mitandao ya kijamii.
Utakapojua mambo haya ya msingi basi utaweza kabisa kujifunza na hatimaye kutengeneza picha zinazovutia sana.
Ni mambo 8 ambayo yatakufungua macho yako.

Sifa bainishi 8 za picha na habari picha zinazopendwa na watu katika mitandao ya kijamii

Kazi ya kuandaa na kuweka picha na habari picha zenye mwonekano mzuri kabisa haipaswi kuwa jambo linaloogofya.
Kuna mambo 8 pekee ambayo unapaswa kuyaelewa.

Sifa ya 1: Picha na habari picha ni lazima ziwe katika kipimo sahihi

Kila mtandao wa kijamii una masharti na mpangilio wa kipimo sahihi cha picha.
Kwa hivyo huwezi kuandaa picha au habari picha yenye kipimo fulani na kudhani kwamba inaweza kukaa vizuri kwa kila mtandao wa kijamii. Ni lazima uhakikishe kuwa picha na habari picha unayoiandaa itaonekana vyema kwa kila mtandao husika.
Kwa nini?
Kwa sababu kama umeandaa picha yenye kipimo cha 940px kwa 780px kwa ajili ya Facebook basi picha hiyo itaonekana kama iliyokatwa kama utaiweka katika mtandao wa Instagram.
Utakuwa unajionesha kuwa hautilii mkazo kile unachokiandika na kukipakia katika ukurasa wako wa biashara. Utaonekana mtu usiyejali kwa kuwa picha na habari picha itapunguza ushawishi wake kwa msomaji.
Na kama mtu ataona kuwa haupangilii mambo yako vizuri unategemea nini? hatakaa muda mrefu kutazama picha au habari picha yenye mwonekano hafifu ilihali kuna zile zinazoonekana vyema kwa watu wengine.
Unaweza kuepuka aibu hii kwa kufahamu nini kinahitajika na kwa kipimo gani. Huu hapa ni mpangilio wa vipimo tofauti vya picha zinazotakiwa kuwekwa katika mitandao ya kijamii:
Twitter
Picha zenye vipimo vya aina 3 zinahitajika katika mtandao wa Twitter; profile photo,header photo, na in-stream photo.
Profile photo inatakiwa kuwa na kipimo cha 400px urefu kwa 400px upana. Na picha hii inatakiwa kuwa yenye ukubwa usiozidi MB 2 na iliyo katika mfumo wa JPG, GIF, au PNG.
1-twitter-profile-photo
Header photo inatakiwa kuwa katika kipimo cha 1500px upana na 500px urefu. Na picha hii inatakiwa kuwa na ukubwa usiozidi MB 5 na iliyo katika mfumo wa JPG, GIF, au PNG.
2-twitter-header-photo
In-stream photo inatakiwa kuwa na kipimo cha 440px upana na 220px urefu. Hii ina maana kwamba urefu na upana unatakiwa kuwa katika uwiano wa 2:1. Picha iwe na ukubwa wa MB 5 na katika mfumo wa JPG, PNG, au GIF.
3-twitter-instream-photo
Facebook
Picha zenye vipimo vya aina 5 zinahitajika katika mtandao wa Facebook; profile photocover photoshared imageshared link image, nahighlighted image.
Profile photo inatakiwa kuwa na kipimo cha 180px urefu kwa 180px upana. Na picha hii inatakiwa kuwa yenye ukubwa usiozidi MB 2 na iliyo katika mfumo wa JPG, GIF, au PNG.
4-facebook-profile-photo
Facebook cover photo inatakiwa kuwa na kipimo cha 828px upana na 315px urefu. Ili upate matokeo mazuri hakikisha unapakia picha yenye ukubwa wa KB 100 katika mfumo wa JPG.
5-facebook-header-photo
Facebook shared image inatakiwa kuwa katika kipimo cha 1200px upana na 630px urefu.
6-facebook-shared-photo
Facebook shared link imageinatakiwa kuwa katika kipimo cha 1200px upana na 627px urefu.
7-facebook-shared-link-photo
Facebook highlighted imageinatakiwa kuwa katika kipimo cha 1200px upana na 717px urefu.
8-facebook-highlighted-photo
Instagram
Mtandao huu unatumia kushirikishana picha kama mfumo mzima wa biashara. Itakupasa kuandaa picha za aina tatu: profile picture, photo thumbnails, na picha yenyewe.
Instagram Profile photoinatakuwa kuwa katika kipimo cha 110px urefu na 110px upana.
9-instagram-profile-photo
Instagram thumbnail photoinatakuwa kuwa katika kipimo cha 161px urefu na 161px upana.
10-instagram-tumbnail-photo
Tumbnail photos ni picha zilizo katika mpangilio wa safu (rows and columns) ambazo huonekana pale mtu anapotembelea ukurasa wako wa Instagram. Picha hizi zitatanuka pale mtu anapobonyeza kwa kutumia kipanya.
Instagram photo ndizo zinatakiwa kuwa katika kipimo cha 1080px urefu na 1080px upana.
11-instagram-photo

Sifa ya 2: Picha na habari picha lazima zijibainishe sawasawa – zinatakuwa kuwa bora sana

Watu wanapakia picha na maandiko mengine mengi kwa mwendokasi mkubwa sana.
Kama unataka uonekane miongoni mwa mamilioni ya picha, habari picha, na maandiko mengine katika mitandao ya kijamii basi lazima uandae picha nzuri kupindukia.
Ni lazima uandae picha ambazo zitakuwa na mvuto mkubwa sana katika macho ya watu. Lengo lako lazima liwe, “Ninawezaje kuwafanya wasomaji kuacha kushuka chini katika kurasa zao na kuamua kutazama na kusoma kile nilichoandika?”
Vigumu?
La hasha. Ni rahisi tu kama utajua nini unafanya na lengo lako ni nini. kwa mfano, tazama kwa makini picha mbili hapa chini:
12-bad-photo
Picha kama hii haitapata wafuasi wengi. Haina mvuto wowote
13-good-photo
Picha kama hii bila shaka itakufanya utulie kutazama. Utaanza kujiuliza, nini kimetokea hapa?
Ili kuandaa picha inayofikirisha na kuwafanya watu wa LIKE, ku SHARE au ku COMMENT tumia dondoo hizi:
  • Achaana na wazo la kutumia picha mbazo tayari zimekwisha tumika. Hasa picha ambazo zinapatikana katika tovuti za kuuza picha na ambazo zina mwonekano wa kiofisi na ‘kikampuni’ zaidi.
  • Jiulize, “Je, picha hizi zinaendana na mada au maudhui ya kile ninachofanya?
  • Hakikisha picha na habari picha ina mwonekano bayana katika macho ya watazamaji
  • Chagua picha na habari picha zinazoonekana vizuri na rahisi kutoa ujumbe kwa hadhira
  • Usiingie katika mkumbo kwa kufanya yaleyale ambayo wengine wanafanya katika kurasa zao za biashara za mitandao ya kijamii.

Sifa ya 3: Picha zinazoonesha watu ni lazima zioneshe nyuso zao bayana, hasa wakiwa wanatabasamu

Watu huvutiwa na watu wengine.
Watu ambao sisi huwapenda na kuvutiwa nao ni watu ambao hutabasamu muda mwingi. Jaribu kutembelea kurasa za biashara za mitandao ya kijamii kujifunza nini hasa wanafanya.
Tazama kurasa kama benki ya CRDB na Whitedent Tanzania.
14-tabasamu
15-tabasamu
Unapoandaa picha au habari picha zinazoonesha watu, hakikisha wanakutazama wewe. Picha itatoka ikiwa na mwonekano wa kumtazama yule anayekuangalia.
Picha zote mbili hapo juu zina mvuto kwa sababu wahusika ni kama vile wanakutazama moja kwa moja.

Sifa ya 4: Tumia hashtags na mbiu (slogas)

Picha na habari picha ni njia nzuri sana ya kuanzisha mazungumzo.
Mazungumzo katika mitandao ya kijamii ni namna watu wanavyotoa maoni juu ya kile kilichoandikwa. Kama utaweka picha inayofikirisha na kuvutia, basi bila shaka watu watapenda kutoa maoni yao.
Kama utaweza kuwashawishi watu wazungumze juu ya picha na habari picha basi watakuwa tayari kutazama na kubarizi bidhaa au huduma unazotoa.
Linapokuja swala la kuchagiza mazungumzo, basimbiu na hashtags ni visaidizi vikubwa kwako.
Bila shaka umewahi kuona hashtags kama vile#bringourgirlsback katika kusaidia kuhamaisha watu kuwakomalia wana mgambo wa book harama kuwaachia huru wasichana waliowateka huko Nigeria.
Utaona mtu kama Madonna akitumia hashtag hii kuwahamasisha watu kupiga kelele juu ya kadhia hii.
16-mbiu
Unaweza kuona watu 51,000 wame LIKE, watu 2100 wametoa maoni na watu 15,000 wamesambaza ujumbe huu.
Utaona kwamba Madona kamtumia binti kutoka India ambaye alihamia Uingereza baada ya watu wenye siasa kali kutaka kumuua kwa sababu alipigania haki za wasichana kupata elimu.
Utaona hashtags kama vile#ShareaCoke kutoka kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola inavyowahamisha watu kushirikisha stori zao kwa kile wanachokunywa.

Sifa ya 5: Tumia manenomsingi (keywords) katika picha au habari picha

Katika lugha ya kidijitali kuna maneno maalum yanayotambulisha msisitizo wa kile kinachozungumzwa. Haya yanafahamika kama keywords.
Unapotumia maneno haya, unakuwa na uwezo wa kutambua hadhira na kuifanya ikutazame kwa makini. Ni kama vile kuwaambia, “Hey, jamani, nipo hapa. Nisikilizeni.”
Maneno haya ni yale ambayo unadhani wasomaji wanajihusisha nayo katika maisha ya kawaida. Kwa mfano, neno ajira, kazi, ujasiriamali, biashara, n.k yanatumiwa sana.
Kama unaandaa picha na habari picha juu ya bidhaa au huduma basi lazima utumie maneno maalum katika maelezo ya picha hizo. Unapoambatanisha maneno haya unakuwa unahakikisha kwua wahusika wataziona na kuzisoma picha au habari picha husika.
Maneno unayotumia lazima yakamilishe mambo yafuatayo:
  • Ni lazima yawavutie wasomaji na kuwafanya kuweka umakini
  • Ni lazima yawafanye wasomaji kuendelea kusoma maudhui husika inayohusiana na picha au habari picha
  • Ni lazima yawashawishi wasomaji kwamba kuna faida fulani ndani kama wataendelea kusoma
Haya yote yatapelekea wewe kupata mrejesho wa watu. Watu watabonyeza vitufe vya vipanya vyao zaidi.

Sifa ya 6: Picha na habari picha zenye mafanikio siku zote huwa na mwendelezo katika muonekano

Ni lazima ujitofautishe kama unataka kufahamika mara tu msomaji anapokuona.
Picha na habari picha lazima ziwe na muonekano tambulishi ambao kila mtu ataufahamu mara moja. Hii ni kuweka mtindo wa rangi, maneno, na mtazamo mzima wa picha na habari picha kwa namna ambayo inasema waziwazi, “huyu ni Afrilife.”
Unafanikisha hili kwa kuchagua rangi ambayo ndiyo itatumika kukutambulisha kuwa wewe ni mjasiriamali au mfanyabiashara fulani. Kisha unachagua aina ya muundo wa herufi (fonts) ambao unakutanabaisha vizuri.
Kwa mfano, utaona kuwa Tigo huweka picha zenyeusuli (background) wenye rangi ya bluu na maandishi meupe katika font ya aina yaFertigo Pro.
17-image-consistent
Au kampuni kama airtel picha na habari picha huwa zina mwonekano wa usuli mweupe, nembo ya kampuni upande wa juu kushoto na maandishi yenye rangi nyeupe katika kiboksi chekundu:
18-image-consistent
Unawezaje kuifanya picha na habari picha kuonekana yenye mwendelezo na mwonekano sawia siku zote?
Kuna dondoo kadhaa kama zifuatazo:
Tumia kile kinachofahamika kama filters (kama chujio kwa ajili ya kukoleza au kufifisha rangi) katika picha. Filters hizi ziwe ni zilezile katika picha zote unazoandaa.
Tumia fonts zilezile katika maandishi yako ndani ya picha. Kama umemaua kuchagua font aina yaVerdana basi itumie hiyohiyo siku zote.
Tengeneza na jenga mtindo wa mwonekano wa utambulisho wa biashara yako na endelea kuukumbatia
Hakikisha unachagua rangi utakazozitumia siku zote katika biashara yako na usichepuke hata kidogo katika kuzitumia
Weka chapa (watermark) – nembo, hashtag, au mbiu katika kila picha. Tazama picha za Tigo au Airtel, unaona nini?

Sifa ya 7: Picha na habari picha ni lazima zihusiane na utambulisho wa biashara na hadhira yako

Kama unauza kuku na ukaweka picha zinazohusiana na samani, basi hapo unachepuka sana. Hadhira yako haitakuelewa. Na kwa vyovyote hautakuwa unajitangaza vyema kibiashara.
Picha na habari picha unazozitumia lazima ziakisi kile unachokifanya. Ni lazima kiendane na matarajio ya hadhira yako. Wateja wanataka nini?
Hebu tembelea ukurasa wako wa Facebook, Twitter, au Insatgram. Unaona nini?
Je,
  • Picha na habari picha zinahusiana na biashara, hadhira, na utambulisho wako kama fulani?
  • Picha na habari picha zinahusiana na tasnia ya biashara uliko?
  • Ni dhahiri (kwa kutazama picha au habari picha) kwa mtu kutambua ni bidhaa au huduma zipi unazozitoa?
Endapo picha na habari picha unazotumia katika mitandao ya kijamii hazioani na ujumbe, malengo, una tambulisho wa biashara yako kwa ujumla basi utakuwa unawachanganya wateja.
Wateja au wafuasi wako hawatakaa muda mrefu katika kurasa zako.

Sifa ya 8: Habari picha na picha zinaweza kuwavutia wasomaji hata kama ni maandishi ndani ya maumbo yenye rangi

Si lazima upige picha.
Si lazima ununue picha kutoka kwa mitandao kamawww.stockphoto.com auwww.gettyimages.com.
Unaweza kabisa kutumia kile kinachofahamika kama text based images. Hizi ni rahisi sana kuziandaa na zinapendwa na watu wengi.
Hupendwa na watu wengi kwa sababu zifuatazo:
  • Unaweza kushirikisha watu wengine juu ya nukuu mbalimbali katika kuhamasisha au kukumbusha
  • Unaweza kutoa ujumbe fulani
  • Unaweza kuwahamasisha watu kubonyeza picha husika kwa kuandika maneno yanayofikirisha na kujenga hamu ya kutaka kujua zaidi
  • Unaweza kutengeneza picha ambayo inaweza kubonyezwa kuelekea mahali pengine katika tovuti
  • Unaweza kusisitiza thamani ya ofa au bidhaa au huduma kwa kutumia picha au habari picha
19-text-based-images
Mfano wa text based image kutoka success swahili
Tumia dondoo hizo hapo juu kuandaa habari picha. Chagua mojawapo ya hizo, si lazima uzitumie zote. Tazama ni kwa kiasi gani zinawafanya watu wazungumze nawe au kupata LIKES nyingi zaidi.
Itaendelea …