Kila mmoja anatamani mafanikio, lakini wengi wetu tunatamani mafanikio. Hatuyapati kwa sababu hatuchukui hatua, hatufanikiwi kwa sababu hatuna utashi na nia ya kujaribu kwa nguvu na akili zote katika kuyapata mafanikio hayo.
Kuna sababu nyingi kwa nini watu wengi hawafanikiwi  japo wengi wanaishi wakitamani siku moja wafanikiwe. Katika andiko hili utafahamu sababu mbili kati ya zile muhimu zinazofanya wengi wasifikie mafanikio wanayoyatamani.

Elimu na mtazamo

Elimu ni kitu kizuri sana, inafungua uwezo wetu wa kuyaelewa mambo haraka. Lakini vilevile elimu tunayoipata mashuleni inatuingizia kanuni fulani katika akili zetu ambazo tusipokuwa makini zinakuwa kikwazo kwetu kujifunza mambo mapya au kufiri vinginevyo.
Mfanyabiashara mashuhuri duniani na muelimishaji Bw. Strive Masiyiwa anasema “kwa yule aliyefundishwa tu kutumia nyundo, kila tatizo huwa ni msumari” .
usemi-wa-masiyiwa
ELIMU INAWEZA KUWA KIKWAZO KATIKA MAFANIKIO YAKO
Watu walio wengi wakipata elimu ya taaluma fulani, basi hujaribu kupata majawabu ya kila kitu ndani ya taaluma hiyo.
Mfano:
  • Daktari hujaribu kutafuta jawabu la kila tatizo la afya kwa kutumia dawa,
  • Bingwa wa upasuaji hujaribu kutibu kila ugonjwa kwa upasuaji,
  • Mwanasheria hujaribu kutafuta jawabu la tatizo mmomonyoko wa maadili au matatizo ya ndoa kwa kutumia mfumo wa kisheria na
  • Mchumi hujaribu kutatua matatizo hayo kwa njia au nadharia za kiuchumi.
Hivyo hivyo watu wanapotafuta njia za kujikwamua kiuchumi hutafuta fursa ndani ya miktadha wa taaluma zao.
Kwa mfano daktari atafungua kliniki binafsi, mwanasheria atafungua ofisi ya uwakili, mwalimu ataanzisha kufundisha masomo ya ziada (tuisheni),mchumi au mhasibu atafungua ofisi ya ushauri wa kitaaluma au atatafuta mwajiri mwingine anayelipa zaidi ya yule aliye naye na siku hizi wengi wanafikiria kuingia kwenye siasa.
Lakini hebu tuone mfano mmoja hai wa hapa Tanzania.
Bw. Reginald Mengi ambaye ni mfanyabiashara mkubwa hapa nchini, licha ya kwamba alikuwa ni bingwa wa taaluma ya uhasibu alianza safari yake ya biashara kwa kuuza kalamu za Bic.
Kwa hiyo ukitaka kusonga mbele lazima ufikiri nje ya boksi na uwe tayari kujifunza mambo mapya.
Vilevile mitizamo yetu ya maisha inajengwa na mambo tunayoyasikia kila mara, tunayoyaona kila mara, tunayoyawaza kila mara, tunayoyahisi kila mara n.k. hivyo kuna baadhi ya mitizamo au imani zilizokwishajengeka akili mwetu ambayo ndio kikwazo kwetu kupiga hatua.
Kwa mfano mara nyingi utasikia watu wakisema ‘sisi wenye nywele ngumu hatuwezi’ au ‘wazungu wana akili nyingi’ au ‘mwanamke ataweza nini’ au ‘ biashara wanaziweza watu wa kabila fulani’ nk. Lakini vile vile kuna kile tulichoaminishwa na jamii kuanzia wazazi wetu, wajomba, majirani, walimu , marafiki kwamba tukisoma tukapata kisomo kizuri hatimaye tutapata kazi nzuri na kwamba kazi nzuri ndio maisha mazuri, heshima kwa jamii n.k.
Lakini tukumbuke kuwa mafanikio makubwa hatuwezi kuyapata kwa kuajiriwa , ndio maana hakuna tajiri aliyeajiriwa. Lazima tubadili mitizamo yetu.

Woga

Wataalamu wanataja kuwa kikwazo kingine kikubwa cha mafanikio ni woga. Lakini lazima pia tukubali kuwa woga ni hulka ya binadamu, hivyo kuwa na woga ni kawaida.
Kuna woga wa aina nyingi, mfano woga wa kufanya kitu kipya,woga wa mabadiliko, woga wa kutokubalika kwa ndugu na marafiki, woga wa kukosea, woga wa kushindwa, woga wa kupoteza fedha n.k.
Woga huu wote hujumuishwa pamoja na kuitwa woga wa kisichojulikana.
Watu wengi hushindwa kuchukua hatua ya kuanza mradi au biashara kwa sababu wanataka wawe na uhakika wa matokeo kwa 100% kabla ya kuanza, kitu ambacho hakiwezekani.
Mbaya zaidi huenda kuomba ushauri kwa watu wenye woga kama wao na ambao hawajawahi kufanya hicho wanachotaka kufanya.
Ndio maana sifa mojawapo muhimu sana na ujasiriamali ni kuwa na ujasiri wa kuwa tayari kukabiliana na matokeo yoyote ili kusonga mbele.
Hivyo ili uweze kufanikiwa lazima ukubali kutoka kwenye hali ile uliyozoea watalaam wanaita ‘ukanda wa utulivu’ (comfort zone). Yaani uwe tayari kutokubaliana na walio wengi, kupoteza baadhi ya marafiki,kufanya mambo ambayo hujawahi kufanya, kubadilisha ratiba ya kila siku,kubadilisha baadhi ya mazoea, kujifunza mambo mapya, kutokuwa na visingizio, kuwa chanya n.k .
Hizi ndizo gharama za mafanikio, hakuna mafanikio bila gharama.
Tuchukue mfano wa mtu anayetaka kupata mafanikio kwa kucheza filamu.
Ili aweze kucheza filamu anahitaji kuwa na ujasiri wa kukabiliana na woga wa kuongea mbele ya watu (kamera), woga wa kukosea, woga wa kukataliwa au kudhiakiwa na ndugu na marafiki,woga wa kushindwa, woga kufanya kitu kipya, woga wa kufanya matendo fulani mbele ya kadamnasi, woga wa kuumia kwa michezo yenye hatari, n.k.
Hali ni hiyo hiyo kwa anayetaka nyota wa mchezo fulani au mfanyabiashara mkubwa.Njia ya kupunguza woga ni kurudiarudia kulifanya jambo hadi linakuwa mazoea, na hii inahitaji juhudi na kujitoa haiji kirahisi tu.
Umejifunza nini katika andiko hili? Jadiliana nasi. Acha maoni yako hapa.