Header Ads Widget

Aliyemweka Mtanzania rehani Pakistan akamatwa

MFANYABIASHARA Juma Mwinyi maarufu (Neti)
aliyekuwa akidaiwa kumweka reheni mdogo wake
nchini Pakistani kwa Sh bilioni 1.5 afikishwa
mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha binadamu.
Juma alipanda kizimbani jana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka
yanayomkabili mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian
Mkeha.
Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Peter
Njike alidai kati ya Desemba Mosi mwaka 2015 na
Julai 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam
mshtakiwa alitenda kosa la kusafirisha binadamu
kinyume cha sheria.
Njike alidai Juma alijifanya anakwenda kumpa
mafunzo Adam Akida Mkazi wa Magomeni, Mtaa
wa Chemchem na Idirsa na badala yake
alimsafirisha kwenda nchini Pakistan kwa ajili ya
kumweka reheni.
Mshtakiwa alipotakiwa kujibu kama kweli ama si
kweli, alikana kuhusika na tuhuma hizo na upande
wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo
haujakamilika wakaomba kuahirisha kesi.
Hakimu Mkeha alimfahamisha mshtakiwa kwamba
shauri lake halina dhamana kisheria, anaamini
upande wa mashtaka hautachukua muda mrefu
kukamilisha upelelezi.
Baada ya kusema hayo, alikubali kuahirisha kesi
hiyo hadi Agosti 17 mwaka huu kwa ajili ya
kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.
Hatua ya kukamatwa kwa Juma, ni matokeo ya
gazeti hili kuripoti habari za Mtanzania kushikiliwa
ughaibuni kutokana na biashara ya dawa za
kulevya Julai 18, mwaka huu.
Habari hizo ziliripotiwa baada ya video kusambaa
katika mitandao ya kijamii Julai 17, mwaka huu
ikimwonesha Adamu Akida alivyowekwa chini ya
ulinzi na maharamia hao wenye silaha.
MTANZANIA lilifuatilia tukio hilo na kubaini kuwa,
Adamu alikuwa amewekwa rehani kwa gharama ya
Sh bilioni 1.5 kwa kile kilichoelezwa kuwa ilikuwa
ni utekelezaji wa mpango wa biashara ya ‘unga’.
Kutokana na hatua hiyo, timu ya MTANZANIA
iliamua kuchimbua suala hilo ili kujua ukweli wa
namna kijana Adamu Akida, alivyokuwa kwenye
mateso hayo.
Akisimulia tukio hilo kaka yake aliyejitambulisha
kwa jina la Hemed Abdallah (si jina lake halisi)
alisema miezi minane iliyopita, Adamu alikwenda
kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake
mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma na
kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya
kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa
ngumu.
Alisema baada ya kueleza shida yake, Juma
alimuhoji kama yupo tayari kwa ajili ya kutafuta
maisha nje ya nchi na Adamu alikubali kufanya
kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata fedha.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama
yake mdogo anaitwa Juma na kuomba asaidiwe
mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana.
Baada ya hali hiyo aliambiwa kuna safari ya
kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa
wameandamana watu watatu pamoja na Juma na
kijana mwengine ambaye jina lake limenitoka, ila
anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na
yule kijana wa Kinondoni, huku Adamu akiachwa
Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku tano
atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote
hata tukihoji alipo Adamu tunaambiwa yupo
anaendelea na kazi huko aliko na angerudi mwezi
wa tisa au wa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya
Adamu, maskini sijui kama tutampata akiwa hai.
Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa
tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani
amekuwa na fedha nyingi sana hadi kufikia
kuwajengea nyumba dada zake pamoja na
kuwanunulia magari,” alisema Abdallah huku
akibubujikwa na machozi.
Kutokana na hali hiyo vyombo vya dola vilianza
kuendesha msako wa ndani na nje ya nchi
kumsaka Juma Neti, ambapo kutokana na hali
hiyo ilielezwa kuwa walifika mara kadhaa
nyumbani kwake Kunduchi Unonio kwa ajili ya
kumsaka bila mafanikio, kwani alitoroka.
Mke alivyohama
Julai 19, mwaka huu chanzo cha uhakika
kililiambia MTANZANIA kuwa mke wa Adamu
ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni,
alihamia Kijitonyama.
Mke huyo wa Adamu, alihamishwa na shemeji
yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba
nyingine Kijitonyama.
“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa
Adamu anajua kinachoendelea, maana miezi mitatu
iliyopita alihama Magomeni na kuhamia
Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu
anarejea nchini.
“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa
hata kupatikana hapatikani na hatujui amehamia
nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema Abdallah.
Kauli ya Mwenyekiti wa Mtaa
Akizungumza na Mtanzania, Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Idrissa, Issa Mpangile, alisema askari
kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi walifika
katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda
katika nyumba ya baba mdogo wa Adamu.
Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia
Mtaa wa Idisa, ambaye ndiye baba mdogo wa
Adamu, polisi walichukua maelezo yake na
baadaye wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa
kuchukua maelezo yake.
Akizungumzia kuhusu kijana huyo, Mpangile
alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini
baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na
Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.
Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo,
alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya
kusafiri kwenda nje ya nchi.
Alisema katika mazungumzo na Baharia,
alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana
huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.
Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba
wa kijana huyo anayejulikana kwa jina la Akida,
amesikia habari za mtoto wake na kwamba
atakwenda kuripoti kituo cha polisi.
Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika
kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa
polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu
wanaofika nyumbani kwao kuhoji kuhusu suala
hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.
Inasemekana kijana huyo aliwekwa rehani kwa
ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na
zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa
karibu wa Mtanzania huyo zinasema kuwa, Adamu
aliwekwa rehani na kaka yake aitwaye Juma
akitakiwa kulipa fedha za unga (mihadarati)
aliyochukua.

Post a Comment

0 Comments