Madiwani wa Ukawa wa Manispaa ya Kinondoni
wamesusa kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai
kiongozi huyo hana uhusiano mzuri na viongozi wa
upinzani.
Jana, Makonda aliitisha kikao cha wakuu wa
wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara za manispaa
za Temeke, Ilala na Kinondoni na madiwani wote,
wakiwamo wabunge wanaounda halmashauri hizo.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Arnaoutoglou kililenga kuzungumzia
masuala mbalimbali, kama maeneo yaliyovamiwa
na uboreshaji wa elimu mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, meya wa
Kinondoni, Boniface Jacob alisema Makonda
amekuwa na tabia ya kudharau na kutoheshimu
viongozi wenzake, hasa wa upinzani akiwaona
hawatendi kazi vizuri.
Pia, Jacob alidai kuwa Makonda amekuwa na
tabia ya kuingilia kazi zinazofanywa na viongozi
wengine kwa kutumia cheo cha ukuu wa mkoa,
jambo ambalo meya huyo alisema ni kinyume cha
sheria.
“Akitaka tumpe ushirikiano, Makonda abadilike la
sivyo mtindo utakuwa huuhuu, mambo yatakuwa
hivi. Huu ni mwanzo na ndiyo maana leo (jana)
Ukawa Kinondoni tumekuwa na msimamo mmoja,”
alisema Jacob.
Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo
(Chadema), alisema hawakuona umuhimu wa
kwenda katika kikao hicho kwa sababu kiongozi
wa mkutano huo anawadharau.
Akijibu tuhuma hizo, Makonda alisema madiwani
waliohudhuria kikao hicho maeneo yao yalikuwa na
shida na yanahitaji kushughulikiwa, hivyo si kazi
yake kuhesabu watu na kubaini nani hakufika
mkutanoni.
Alisema ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni
kujadiliana namna bora ya kuvirudisha viwanja
vilivyochukuliwa na kuvirejesha kwa matumizi
yaliyokusudiwa.
“Huyo anayelalamika mwambie huo anaoufanya ni
utoto akikua ataacha. Narudia tena siyo kazi yangu
kuangalia nani hajaja kwenye kikao,” alisema.
Kwenye kikao hicho, meya wa Ilala (Chadema),
Charles Kuyeko alikuwapo kwenye mkutano huo
pamoja na madiwani wenzake, sambamba na wale
wa Temeke.
Makonda si mgeni wa tuhuma .Aliteuliwa kuwa
mkuu wa wilaya ya Kionondoni katika kipindi
ambacho alikuwa akituhumiwa kuhusika kwenye
sakata la kupigwa kwa Waziri Mkuu wa zamani,
Jaji Joseph Warioba kwenye mdahalo wa Katiba
uliofanyika Hoteli ya Blue Pearl.
Katika kipindi hicho, Makonda pia alikuwa
akituhumiwa kumrushia tuhuma za ufisadi Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiahidi kuwa
CCM isingempitisha kugombea urais.
Akitoa majumuhisho ya kikao cha jana kilichoanza
saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, Makonda
aliwataka watu waliovamiwa na kujenga kwenye
maeneo yasiyoruhusiwa, kuanza kubomoa majengo
yao kabla ya Serikali kuwafikia.
Kabla ya kutoa majumuisho hayo, Makonda alitoa
nafasi kwa madiwani wa manispaa hizo kueleza
kero zinazowakabili, hususan zinazohusu ardhi.
“Najua mchakato huu utawagusa hadi vigogo, lakini
mimi siogopi vita kwa sababu ndani yangu
ninaongozwa na Mungu pekee,” alisema Makonda.
Mbali na hilo, Makonda alisema endapo mtendaji
wa ardhi atayebainika kuhusika katika kuchezea
michoro na ramani ili aachie ardhi na kujipatia
fedha, atashughulikiwa kwa mujibu sheria.
Katika hatua nyingine, Makonda amemwagiza
kamishna msaidizi wa ardhi wa Kanda ya Dar es
Salaam, Mathew Nhange kumwambia Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi awaondoe maofisa ardhi na mipango miji
wa Kinondoni na Ilala baada ya kushindwa kutoa
taarifa za kuridhisha katika mkutano huo.
Huku akiwataja maofisa hao wanaotoka Kinondoni
na Ilala, Makonda alisema alishakutana na wakuu
wa idara kwenye vikao vilivyopita, hivyo
alitegemea kuwa watumishi hao wangetoa taarifa
zilizokamilika.
“ Kamishna naomba umwambie katibu mkuu mimi
siwataki watumishi hawa katika manispaa hizi.
Mwambie awatoe na kuwapangia kazi nyingine,”
alisema Makonda.
Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia
kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za
watumishi hao jana.
0 Comments
on