WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
wafugaji wenye mifugo mingi nchini kujiweka
tayari kwa ajili ya kuhamia kwenye maeneo
yatakayotengwa na Serikali katika ranchi
mbalimbali nchini ili waweze kufuga kisasa.
Pia aliwataka wafugaji hao kushirikiana na Serikali
katika kuboresha miundombinu ya maeneo hayo
ikiwemo ujenzi wa visima vya maji na majosho ili
ufugaji wao uwe na tija.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano,
Agosti 03, 2016) wakati alipotembelea kiwanda
cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch
kilichoko wilayani Movomero.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema kitendo cha
wafugaji hao kuhamia katika ranchi kitawezesha
mifugo yao kuwa na ubora kwa sababu aina ya
ufugaji wa sasa ya kutembeza mifugo umbali
mrefu inasababisha ufugaji wao kuwa na tija
ndogo.
Akizungumzia kuhusu uwepo wa kiwanda cha
kuchakata nyama wilayani Mvomero Waziri Mkuu
alisema kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati
ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wafugaji
watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani
hapo.
“Uwepo wa viwanda katika maeneo yetu
utatuwezesha kupunguza matatizo tuliyonayo katika
maeneo yetu ikiwemo suala la migogoro kati ya
wafugaji na wakulima. Viwanda ndiyo
vitakavyotuondoa kutoka katika uchumi wa chini
hadi wa kati,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi na Mshauri wa
kiwanda cha Nguru Hills Ranch, Dunstan Mrutu
alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja
ng’ombe 300, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku
kinatarajiwa kufunguliwa mwezi Desemba mwaka
huu.
Mkurugenzi huyo alisema takriban asilimia 80 ya
nyama itafungashwa na kuuzwa nje ya nchi hasa
Uarabuni kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania
imebainika kuwa na mvuto maalum katika nchi
hizo.
“Mbali na uwekezaji huu wa kiwanda cha nyama pia
tunatazamia kuwekeza katika mnyororo wa thamani
kuanzia kusindika ngozi inayotoka kiwandani hadi
kuzalisha viatu, mikanda na bidhaa zote za ngozi na
kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya
nchi,” alisema.
Mrutu alisema nia yao ni kuitikia wito wa Rais Dk.
John Magufuli wa kutaka viwanda vizalishe viatu
nchini kuanzia vya majeshi na wananchi wote
ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza
kuuza bidhaa hizo.
Aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utatoa
fursa kwa wafugaji na wakulima kuuza majani,
mifugo na mazao ya chakula kama mtama,
mahindi, ambapo tayari wameanza kuhamasisha
jamii za wafugaji na wakulima wa Mvomero,
Ngerengere na sehemu zinazozunguka eneo la
kiwanda kuchangamkia fursa hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameuagiza
uongozi wa wilaya ya Mvomero kufanya mapitio ya
mashamba ili kujua wamiliki wake na kama
hawajayaendeleza wachukue uamuzi wa haraka wa
kuyatwaa na kuyarudisha mikononi mwa Serikali.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akijibu
ujumbe uliokuwa katika mabango yaliyobebwa na
wananchi wa kijiji cha Maji ya Chumvi wilayani
Mvomero waliosimamisha msafara wakati ukitokea
kwenye kiwanda cha nyama.