Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) limemwomba Rais John Magufuli kumshughulikia
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter
Serukamba kwa maelezo kuwa ni ‘jipu’ ambalo limevuruga mjadala wa
Muswada wa Huduma za Habari.
Hayo
yalibainishwa jana Dar es Salaam wakati wahariri wa vyombo vya habari
walipokuwa wakijadili vipengele vya Muswada huo ambavyo vinatakiwa
kufanyiwa mabadiliko kabla ya kupitishwa kuwa sheria kwa kuwa si rafiki
kwa tasnia ya habari nchini.
Mhariri
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari Limited, Absalom Kibanda alisema
Serukamba ni ‘jipu’ na kumwomba Rais aamini hivyo, akibainisha kwamba
kipindi cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella Mukangara walipeleka
hati ya dharura kutaka Muswada huo ujadiliwe vizuri, lakini alikataa
huku akiunga mkono kama ulivyo.
“Kuna sauti ilisikika ikitembea katika mitandao, nikajiuliza ameongea kama Waziri, Ofisa Habari wa Serikali au mtu binafsi?” Alihoji Kibanda.
Kibanda
alimwomba Rais aangalie ni nani wasemao ukweli kati ya wadau wa habari
(wahariri na waandishiwa habari) na mamlaka nyingine za Serikali kuhusu
namna nzuri ambayo Muswada huo unaweza kujadiliwa na kuwa sheria kwa
maslahi ya Taifa bila kukwaza upande.
Aidha,
alibainisha kuwa kuna watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakimsukuma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, ili aridhie mahitaji
yao kwa maslahi binafsi.
Alisema
kwa sasa waandishi wa habari wanafananishwa na wahalifu na kusema hivi
karibuni walichapisha habari kwenye gazeti lao na walikuja kuomba radhi
baada ya kupokea vitisho.
Aliongeza
kuwa Muswada huo ulitakiwa uwekwe vipengele vinavyowachukulia hatua
watu wanaoingilia kazi za vyombo vya habari, kwa kuwa makosa mengi
vinayotupiwa vyombo vya habari vyanzo huwa ni wanasiasa.
Mjumbe
wa TEF, Jesse Kwayu alisema wana wasiwasi na msimamo wa Serukamba, kwa
kuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia Serikali na badala
yake anakuwa kama ni ofisa wa Serikali.
“Wakati akiusoma Muswada huu kwenye Kamati, akihitimisha alisema hakuna uhuru usio na mipaka,” alisema Kwayu.
Alibainisha
kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliyepita, alisikiliza vizuri
mapendekezo ya wadau wa habari na kuyafikisha bungeni yajadiliwe tofauti
na wa sasa ambaye si msikivu.
Alisema
wakati wakiujadili hivi karibuni Dodoma ilifika mahali kukawa na
mvutano mkali kati ya Serukamba na Zitto Kabwe kwa kuwa alikuwa
hajaridhishwa na namna Muswada huo ulivyojadiliwa, kwa sababu wadau wa
habari wahusika hawajahusishwa kikamilifu.
Alisema asilimia 80 ya waandishi wa habari wako mikoani ambako waandishi hao pia hawajajadili na kupata mwafaka wa Muswada huo.
Naibu
Mhariri Mtendaji wa Jamhuri, Manyerere Jackton aliwataka Serukamba na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Hassan Abbas wasijisahau na
kupitisha Muswada huo eti kwa kuwa wako serikalini, bali wajue kuwa kuna
wakati watarudi na kukabiliwa na sheria hiyo.
Mwenyekiti
wa TEF, Theophil Makunga alisema Muswada huo usipobadilishwa vipengele
hivyo na ukapitishwa kuwa sheria, waandishi wa habari watakuwa kwenye
shida kubwa kwa kuwa watakuwa wakipambana na kitu kibaya sana.
0 Comments
on