Header Ads Widget

Bilionea wa Chadema Mustapha Jaffer Sabodo Akitosa Chama Hicho.........Aahidi Kutoa Trilioni 10 za Kuwekeza Dodoma ili Kumuunga Mkono Rais Magufuli

MFANYABIASHARA maarufu, Mustapha Jaffer
Sabodo ametangaza kutoa dola za Marekani bilioni
5 (Sh trilioni 10) kwa ajili ya kuwekeza mkoani
Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais
John Magufuli kuhamisha makao makuu ya
serikali kwenda mkoani humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Sabodo alisema
atawekeza kiasi hicho cha fedha, iwapo serikali
yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza
ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa
makao makuu ya nchi.
Alisema alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda
marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama
mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi
makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono
hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo
aliita ‘Azimio la Dodoma’.
“Niliposikia anatangaza kwenye televisheni ya taifa
kwamba Serikali itahamia Dodoma, ilikuwa mara
yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita,
nilitabasamu moyoni, jambo ambalo lilinitokea
miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius
Nyerere.
“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona ile roho ya
Nyerere imezaliwa tena.
“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la
Dodoma kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 5,
ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa
katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,”
alisema Sabodo.
Sabodo alisema atatoa fedha hizo ili zitumike
kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo,
viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine
ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.
Alisema kuwepo kwa huduma hizo mkoani
Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo kukidhi
matakwa ya watumishi wa umma watakaohamia
huko.
Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa atafanya
uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake ni
kuona mji wa Dodoma, unaungana na miji ya jirani
kama Mpwapwa, Kondoa na Manyoni ili kutoa
fursa ya kupanua huduma mbalimbali katika
makao makuu hayo ya nchi.
Sabodo alisema kwamba juhudi zake za kuwekeza
katika huduma za jamii kama shule, pia
ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha
kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa,
ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa eneo hilo.
Kwa upande wa huduma ya afya, Sabodo alisema
atatumia umaarufu wake kuwashawishi wamiliki
wa Hospitali ya kimataifa ya Apollo ya India ili
waje nchini wakashirikiane naye kujenga hospitali
ya kisasa, ambayo itakuwa inatoa huduma za
kisasa mkoani humo.
“Mnaifahamu hospitali ya Apollo ni wawekezaji
wakubwa katika huduma za afya, kwa kusukumwa
na hatua hii ya Rais nitaongea nao tushirikiane
katika kujenga huduma za jamii katika mji huo,”
alisema Sabodo.
Pia alisema atawashawishi wawekezaji wengine
kutoka nchi za India, Singapore na kwingineko kuja
kuwekeza katika mji huo wa Dodoma katika sekta
ya viwanda, kuhakikisha kwamba azma ya Rais
Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda inatimia.
Sabodo ambaye alisema wazi kuwa utendaji wa
Rais Magufuli, umemvutia kutokana na hatua yake
ya kupiga vita rushwa, alitangaza kuwa kuanzia
sasa hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani
kama ambavyo amefanya miaka ya nyuma kama
njia ya kuimarisha demokrasia nchini.
“Huko nyuma nilikuwa nawapa Chadema fedha
kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuimarisha
demokrasia, sasa natangaza tena kwamba
sitawapa tena fedha, niwape za nini wakati Rais
aliyeko madarakani anafanya kazi ambayo ndio
nilikuwa naipigania?" alihoji Sabodo.
Sabodo ni mfanyabiashara wa kitanzania mwenye
asili ya Kihindi ambaye alizaliwa mkoani Lindi.
Katika maisha yake amekuwa anafanya biashara
katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na
Zimbabwe.
Pamoja na biashara zake, Sabodo amekuwa
anajihusisha kuchangia katika miradi ya maendeleo
ya huduma za jamii, uimarishaji wa demokrasia
nchini na pia alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi
ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha bahati nasibu.

Post a Comment

0 Comments